Na Peramiho Publications
“Namna gani mbona hamwelewi vijana!...... ” ni Maneno ya mzaha au masihara toka kwa aliyekuwa Abate wa tatu wa Abasia ya Peramiho, Emeritus Lambert (Helfried) Dorr (OSB) akiwa darasani na wanafunzi wa utawa, mwaka 2006 (Peramiho).
Uwezo wake wa kupandikiza elimu kwa wanafunzi wengi aliowahi kuwafundisha katika maisha yake wakiwemo wanafunzi wa Likonde pamoja na Abasia ya Peramiho, utakumbukwa daima bila kificho, kwani waswahili wanasema “Kizuri kinajiuza, kibaya kinajitembeza”.
Safari ya maisha ya Padre Lambert ilianza mwaka 1936 katika kijiji cha Gerolzahn kwenye jimbo la Freiburg huko nchini Ujermani. Mwaka 1956 alifanikiwa kufunga nadhiri za muda baada ya kuaminiwa utawani.
Alipata fursa ya kupadirishwa Juni 29, 1960 baada ya kufuzu mafunzo yake vizuri. Alikuja Afrika (Afrika Mashariki) katika viunga vya Peramiho (Tanzania) mwaka 1964.
Akiwa mkoani Ruvuma alianza na kazi ya kufundisha katika Seminari ya Likonde huko Mbinga, kisha Mwaka 1970 alirudishwa Peramiho na aliendelea na kazi yake ya kufundisha katika Seminari ya Peramiho, wanafunzi wa utawa na kazi yake mama ya kutangaza neno la Mungu.
Desemba 08, 1976 alichaguliwa kuwa Abate wa tatu wa Abasia ya Peramiho lakini Kabla ya hapo alikuwa Priori wa Abasia hiyo hiyo ya Peramiho.
Kijiti cha Uabate alikipokea toka kwa Abate Eberhart Spiess OSB, huku Abate wa kwanza wa Abasia ya Peramiho akiwa ni Gallus Steiger OSB.
Lambert alipewa nafasi ya kuwa Abate wa Abasi ya Peramiho isyokuwa na kikomo, lakini yeye baada ya kufanya kazi hiyo kwa miaka 30, mnamo mwaka 2006 aliamua kustaafu na kupisha nguvu mpya kwenye kiti hicho.
Kabla ya yeye kurudi Ujerumani mwaka 2015, baada ya kustaafu alienda kupumzika katika Monasteri ya Tororo (Uganda) kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu kisha mwaka 2008 akarudi Peramiho.
Awali Abate Lambert alipanga kuwa akifa azikwe Tanzania katika makaburi ya Abasia ya Peramiho hata hivyo kutokana na kusumbuliwa na mguu wake wa kushoto kwa muda mrefu madaktari walimshauri kwenda kupata matibabu nchini kwake Ujerumani kwa kuwa Tanzania hakuna hospitali inayoweza kumtibu.
“wakati wowote kabla ya mwisho wa mwaka huu natarajia kurudi nyumbani kwangu Ujerumani kwa ajili ya matibabu ya mguu wangu wa kushoto hivyo kwa kuwa matibabu hayo ni endelevu siwezi kurudi tena Tanzania’’,alisema Abate Lambert mwaka 2015.
Januari 04, 2015 akaagwa rasmi na waumini wa Parokia ya Peramiho katika kipindi ambacho wengi wao bado walikuwa wakiuhitaji msaada wake.
Abate Lambert alikuwa mwalimu wa somo la Historia ya Kanisa katika Seminari ya (Likonde) Kigonsera tangu mwaka 1964 amewafundisha viongozi mbalimbali wa Kanisa na serikali wakiwemo Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Songea Mhashamu Norbert Mtega.
Kabla ya roho yake kuhitimisha safari yake ya hapa duniani Oktoba 22, 2017; mapema mwaka huu, akiwa nchini Ujerumani alipelekwa kwenye nyumba ya Wagonjwa katika Monesteri ya Munsterschwarzach kwa ajili ya matibabu zaidi. Hakika kazi ya Mungu haina makosa, Pumzika kwa amani Abate Lambert!
Moja ya watu ambao wameshtushwa na kifo chake ni Mwanafunzi wake Mtawa Fredrick Mwabena OSB aliyekuwa mwanafunzi wake wa Utawa toka mwaka 2006 hadi 2009 na amefafanua yafuatayo:
“Abate Lambert Dorr OSB, Apumzike kwa Amani. Babu na Mwalimu Wangu, wenyewe tulizoea kumwita Walking Encyclopedia maana alikuwa msomi wa kweli kweli”.
“Kazi yake ya kuiendeleza Abasia ya Peramiho itakumbukwa daima hasa kuanza kuwapokea watawa wazalendo/Africans, 1982 suala ambalo halikuwepo kabla yake na kipindi hicho kilikuwa kigumu sana kwa watawa wazungu na waafrika kukaa nyumba moja lakini yeye alifanikiwa kuukata mzizi huo wa fitina”.
“Lambert alipenda watu wasome, kuna kipindi kuna Mtawa mmoja aliomba kwenda kusoma lakini utawala ulimcheleweshea majibu yake, akaamua kujifungia ndani siku tatu. Taarifa zilipomfikia Abate Lambert siku ya pili yake akapewa ruhusa ya kwenda shule”.
“Lambert alikuwa mtu wa Sala, alikuwa mtu wa masihara, aliwapenda watu wa aina zote bila kuwabagua, alikuwa muwazi, vile vile alikuwa mshauri wa mambo ya taaluma hapa Tanzania”.
“Aidha namkumbuka Lambert alikuwa na sauti nzito sana, hapo Kanisani kwetu zile maiki hazikuwa na msaada kwake alikuwa na uwezo wa kuongea kwa sauti kubwa mno.
Mwisho alikuwa mpenzi sana wa kuvuta Kiko” alisimulia kwa masikitiko makubwa, Bro. Frederick Mwabena OSB.
Vile vile Kat. George Milinga alifafanua kwamba kifo cha Abate Lambert kimeliachia Kanisa pengo kubwa mno kwa kuwa amelifanyia mambo mengi mazuri:
“Yeye ametunza yatima wengi sana, nyumba nyingi za kitawa Kenya, Tanzania na Uganda zilijengwa na kufunguliwa wakati wa uongozi wake”.
“Alitumia fedha nyingi katika ujenzi wa Makanisa mfano Kanisa la Mbinga Mharule na kuwasaidia Mapadre na Makatekista na wakristo wengine; aliupenda upadre wake, utawala wake na mtu wa kutoa mahubiri yenye ujumbe mzito
”.
“Yeye alikuwa msomi na mwandishi wa vitabu vingi vya historia, vile vile alikuwa mwalimu wa somo hilo. Alikuwa mwanzilishi wa watawa waafrika wa kiume ambao tunawaona. Kabla yake walikuwepo watawa Wabenediktine Wamisionari wazungu tu!”.
“Yeye hakupenda makuu, aliishi na waafrika vizuri bila majivuno na alikuwa baba wa wote” anasisitiza mzee Milinga”.
Abate Lambert Yeye ni Msomi wa hali ya juu, alisoma Seminari Kuu ya Saint – Etienne na Voicebook, vile vile alipokuwa kwenye maandalizi ya kuja Afrika yeye na Padre Bonifaz Dinkel walipata fursa ya kwenda kusomea (Historia ya Kanisa) nchini Canada.
Atazikwa tarehe 27, 2017 siku ya Ijumaa huko Ujermani, wakati nchini Tanzania Tarehe 26, siku ya Alhamisi, Kanisa la Abasia ya Peramiho litafanya Misa maalum ya kumwombea.
“Kwa Maana huyu alionekana anampendeza Mwenyezi Mungu, akachukuliwa”
SOLI DEO HONOR ET GLORIA-KATIKA YOTE MUNGU PEKE YAKE ATUKUZWE.