Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa ujumbe wa Kwaresma wa mwaka 2018 ndani yake likitoa msimamo kuhusu masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.
Ujumbe huo ulioandikwa na maaskofu wote 35 wa TEC wakiongozwa na Rais wake, Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa upo katika kitabu cha kurasa 20 ikiwa ni maandalizi ya ibada hiyo ya siku 40, kipindi ambacho ni cha mfungo wa sala kukumbuka siku 40 za Kristo kufunga na kwenda jangwani.
Hali ya kisiasa
Katika ujumbe huo, TEC imesema uamuzi wa Serikali kuzuia maandamano, mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ni kwenda kinyume cha Katiba ya nchi.
Baraza hilo pia limeonya hatua ya Serikali kuvibana vyombo vya habari ikiwa pamoja na kuvifungia kwa sababu mbalimbali.
“Kufungiwa huku kwa vyombo vya habari kumeenda sambamba na kuminya uhuru wa Mahakama na Bunge kwa njia ya kuminya haki wabunge na kutowapa nafasi ya mikutano ya hadhara kama haki yao ya msingi ya kikatiba.”
Alipopigiwa simu ili kutoa maoni ya upande wa Serikali kuhusu ujumbe huo, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema, “Sijaliona bado tamko husika kwa hiyo siwezi kujibu hoja ambayo sijaisoma kwa sasa.”
TEC imetoa ujumbe huo katika kipindi ambacho vyama vya siasa, hasa vya upinzani vikilalamika kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara baada ya Serikali kuipiga marufuku mpaka mwaka 2020, isipokuwa kwa wabunge walioshinda uchaguzi ambao wameruhusiwa kufanya mikutano kwenye majimbo yao.
Ugumu huo umetajwa na vyama hivyo kwamba unapunguza nguvu ya ushindani kwa vyama vya upinzani kukikabili chama tawala.
“Kikatiba, nchi yetu inafuata mfumo wa demokrasia ya vyama vingi. Katiba na sheria mbalimbali zimeainisha utaratibu wa kazi na shughuli za vyama vya siasa. Ili kuhakikisha kwamba shughuli za vyama vya siasa zinakuwa endelevu, vyama vyenye kukidhi vigezo hupewa ruzuku kupitia bajeti ya Serikali inayopitishwa na Bunge,” unaeleza ujumbe huo.
“Hata hivyo, shughuli za, siasa bado zinaendelea kuzuiwa kwa kutumia vyombo vya dola. Maana yake ni kwamba shughuli za kiuenezi za vyama vya siasa, kama vile mikutano ya hadhara, maandamano, makongamano, mijadala na hata mikutano ya ndani, ambayo ni haki ya kila raia, zimekoma mpaka uchaguzi mwingine. Kisheria, huu ni uvunjifu wa Katiba na sheria za nchi.”
Kuhusu vyombo vya habari, TEC imesema Serikali imepunguza wigo wa uhuru wa wananchi wa kupata habari na maoni ya kujieleza na kueleza kwamba kwa ujumla wake, mazingira hayo yatasababisha jamii kufarakana na hata kujenga chuki.
“Kumekuwapo pia hali ya vurugu katika chaguzi mbalimbali. Chaguzi hizi zinaacha nyuma uchungu, hasira, tamaa ya kulipa kisasi na hata kususia chaguzi nyingine,” unasema ujumbe huo wa TEC na kuonya kuwa kama hali hiyo itaachwa, itakuja kusababisha mifarakano mikubwa itakayobomoa amani na umoja wa kitaifa.
Kiuchumi
Kuhusu uchumi, TEC imetoa mambo sita ya kujiuliza; “Tunazitumiaje mali na rasilimali nyingine tulizokabidhiwa na Mungu kama mawakili wake? Tunalipa kodi stahiki kwa ajili ya kugharamia huduma za jamii ambazo Serikali inapaswa kutoa kwa ajili ya wananchi?”
“Wale ambao tu waajiri, tunawajali wafanyakazi na wahudumu wetu kwa kuwalipa mishahara ya halali? Wale ambao tu wafanya biashara, tunalipa kodi zote kihalali?”
“Wale ambao tumepewa jukumu la kukusanya kodi, ushuru na ada nyingine kama tunafanya hivyo kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu husika? Tunaepukaje na kishawishi cha rushwa, hongo, mulungula, magendo au aina yoyote ya ufisadi?”
Kijamii
Katika eneo la kijamii TEC imesema bado kuna kishawishi cha kupingana na azma ya kuboresha maisha ya kijamii.
“Hii inajidhihirisha kwa njia ya uhasama, ugomvi, ukatili kwa watoto na wanawake, ujambazi, na maovu mengine kama hayo miongoni mwa jamii yetu. Kama wamisionari tunaopaswa kuleta habari njema kwa ndugu zetu, kwa nini turuhusu roho ya namna hii ambayo kwa kweli ni roho ya Kaini inayouliza kwa jeuri kabisa,” unasema ujumbe huo.
Mambo matatu
Katika ujumbe wake, Baraza hilo limesema, “Kwa mwaka huu wa 2018 kipindi hiki ni cha kujitafakari mbele ya Mungu na kufanya toba hususan uhai wa amani yetu kwa njia ya matendo ya huruma, haki upendo na amani kwa jirani zetu.”
Limesema hiki ni kipindi chenye upekee wa aina yake kwake sababu ya mambo matatu;
“Ni katika mwaka huu ambapo Kanisa Katoliki Tanzania linaadhimisha na kusherehekea miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, na kilele chake kitakuwa tarehe 2 Oktoba.
Mwaka huu pia utakuwa ni mwaka wa 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania watoe tamko rasmi kuhusu mwelekeo na hatima ya nchi yetu na Mwaka huu ni mwaka wa maandalizi ya utekelezaji wa haki ya msingi ya kidemokrasia ya raia wote ya kuchagua viongozi
wa Serikali zetu za mitaa, vijiji na vitongoji hapo mwakani 2019.”
Kwa sababu hizo tatu, TEC imesema, “Ni vyema tafakari yetu ya Kwaresima ikalenga katika swali ambalo, kwa namna moja au nyingine, linahusu sababu hizo tatu. Kwa njia ya swali hilo mwanadamu hudiriki kumhoji na kumuuliza Mungu na Muumba wake kuhusu hali ya binadamu mwenzake. Swali hilo ni Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” (Mw. 4:9).